Friday, 29 April 2016

Mvua kubwa: Mafuriko Tanzania na Kenya

Leo imekuwa siku ngumu sana kwa uchukuzi mjini Dar es Salaam, Tanzania.
Kisa na maana,,,,mafuriko.

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha hivi sasa kanda yote ya Afrika Mashariki imesababisha mafuriko makubwa ambayo muundo msingi wa barabara za miji ya Nairobi na Dar es Salaam haziwezi kumudu.
Magari ambayo yalijaribu kutumia mabarabara ya Dar es Salaam yalikwama mengine huku yale yenye kimo cha juu yakifaulu kupita

Tuesday, 26 April 2016

Lucy Kibaki afariki

Aliyekuwa mke wa rais wa zamani nchini Kenya Lucy Kibaki amefariki. Lucy alifariki katika hospitali ya Bupa Cromwell mjini London. Alisafrishwa hadi mjini Landon wiki moja iliopita kwa matibabu.Akithibitisha kifo chake rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema kuwa kenya imesikitishwa na kifo cha mama Lucy mke wa aliyekuwa rais wa Kenya Mwai Kibaki.Katika taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari Uhuru amesema bi Lucy amekuwa mgonjwa kwa kipindi cha mwezi mmoja .Amesema kuwa Kenya imempoteza mwanamke aliyechangia mengi katika maendeleo ya taifa la Kenya hususan katika vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.Rais ametuma risala za rambi rambi kwa mtangulizi wake Mwai Kibaki pamoja na familia yake.

Monday, 25 April 2016

Obama akataa pendekezo la Korea Kaskazini

Rais wa Marekani Barack Obama amepuuzilia mbali pendekezo la Korea Kaskazini la kuitaka Marekani isitishe mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Korea Kusini.
Korea Kaskazini imesema itasitisha mpango wake wa kufanyia majaribio silaha za kinyuklia iwapo Marekani itasitisha mazoezi hayo ya kila mwaka.
Akiongea na wanahabari Jumapili, Bw Obama alisema Marekani haichukulii pendekezo hilo kwa uzito na Pyongyang "itahitajika kufanya zaidi kushinda hilo”.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Korea Kaskazini Ri Su-yong ndiye aliyetoa ofa hiyo kwa Marekani wakati wa mahojiano nadra sana na wanahabari.
Mazoezi ya kila mwaka ambayo hufanywa na Marekani na Korea Kaskazini kila wakati huongeza uhasama baina ya nchi hizo mbili na Korea Kaskazini.
Bw Ri alikuwa akizungumza muda mfupi baada ya taifa lake kutangaza kwamba lilikuwa limefanikiwa kufyatua kombora la masafa marefu kutoka kwa nyambizi yake baharini.
Umoja wa Mataifa ulishutumu majaribio hayo ukisema ni ukiukaji mkubwa wa maazimio ya awali ya umoja huo ya kuzuia mipango ya Korea Kaskazini kuwa na silaha za nyuklia.

Friday, 22 April 2016

Donald Trump kubadili sifa zake

Mgombea wa urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump ameahidi kubadilisha sifa zake katika mkutano wa faragha na viongozi wa Republican.
Mfanyibishara huyo ambaye yuko kifua mbele katika kuwania urais kupitia chama hicho alitoa ujumbe wake kupitia wasaidizi wake ,kulingana na chombo cha habari cha AP.
Kuimarika kwake katika mchujo huo kufikia sasa kumetuma ishara miongoni mwa viongozi wa chama hicho kwamba matamshi pamoja na sera zake huenda zisiwavutie wapiga kura.
Majimbo matano yanapiga kura siku ya Jumanne kumchagua mgombea wao wa urais.
Bwana Trump ana uongozi mkubwa wa idadi ya wajumbe lakini huenda asipate wajumbe 1,237 anaohitaji kushinda mchujo huo bila ya mkutano wa wanachama.
Wasaidizi wamewaambia viongozi wa chama kwamba amekuwa akibadilisha sifa zake na kwamba hatua hiyo imeanza kufua dafu.

Monday, 18 April 2016

Korea Kaskazini kulipua bomu la nyuklia

Korea Kusini imesema imepata dalili kwamba Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la tano la bomu la nyuklia, Rais Park Geun-hye amesema.
Hakufafanua zaidi kuhusu dalili hizo, lakini ameagiza jeshi la nchi yake kuwa tayari, shirika la habari la nchi hiyo limesema.
Kumekuwa na ripoti katika vyombo vya habari nchini Korea Kusini kwamba kumeongezeka shughuli katika kituo cha majaribio ya silaha za nyuklia cha Korea Kaskazini cha Punggye-ri, ambapo majaribio ya awali yalitekelezwa.
Iwapo Pyongyang itaendelea na kufanyia majaribio bomu la nyuklia, basi itakuwa ni kukaidi zaidi vikwazo vikali ilivyoongezewa na Umoja wa Mataifa mwezi jana.
"Tupo katika hali ya kutatanisha, hatujui iwapo Korea Kaskazini inaweza kufanya uchokozi kama njia ya kujitetea kutokana na kutengwa na jamii ya kimataifa na pia kuimarisha uungwaji mkono ndani ya nchi,” Bi Park aliambia maafisa wake wakuu wa jeshi, shirika la habari la Yonhap liliripoti.

Sunday, 17 April 2016

Harmonize alivyotoa Burudani ya nguvu kwa watu wa Mwanza kwa mara ya kwanza

Usiku wa April 16, 2016, watu wangu waMwanza kwa mara ya kwanza kwenye stage Harmonize alikutana na watu wake kwenye shangwe na zile hits zake zaBadoAiyola na nyingine, ikiwa ni mwimbaji wa kwanza kutambulishwa kwenye lebo ya WCB inayomilikiwa na mwimbaji wa bongofleva Diamond Platnumz.


Saturday, 16 April 2016

Barabara ya kwanza ya juu kujengwa Dar-es-Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, eneo la Tazara Jijini Dar es salaam ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2018.
Sherehe ya uzinduzi wa mradi huo imefanyika kando ya eneo la makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela Jijini Dar es salaam, ambapo pamoja na Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Mameya wa Jiji la Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida.
Barabara hiyo ya juu itakuwa ya kwanza kujengwa hapa nchini na ujenzi wake umepangwa kugharimu takribani shilingi Bilioni 100 ambapo kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 93.44 zitatolewa na Japan kupitia Shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA), na Serikali ya Tanzania itatoa shilingi Bilioni 8.3.
Barabara ya juu itakayojengwa itakuwa na njia nne na urefu wa mita 300 kutokea maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es salaam kuelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, na inatarajiwa kupunguza kero ya msongamano wa magari yaendayo na yatokayo Uwanja wa ndege na Bandari ya Dar es salaam.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema barabara hiyo inajengwa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya serikali yake ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari Jijini Dar es salaam, ambao kwa mwaka 2013 pekee utafiti umeonesha ulisababisha upotevu wa shilingi Bilioni 411.55
Rais Magufuli amebainisha juhudi nyingine za kukabiliana na msongamano wa magari Jijini Dar es salaam kuwa ni pamoja na kujenga barabara ya njia sita ya Dar es salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na Flyover tano, ujenzi wa barabara nyingine za juu katika makutano ya barabara za Nelson Mandela, Morogoro na Sam Nojuma eneo la Ubungo na ujenzi wa daraja jipya la Salander lenye urefu wa kilometa 6.23 kuanzia Coco Beach hadi hospitali ya Agha Khan.
Juhudi nyingine ni ujenzi wa awamu ya pili wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika barabara za Kilwa, Chang'ombe na Kawawa, na ujenzi wa awamu ya tatu wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika barabara za Nyerere - Gongo la Mboto na Uhuru - Azikiwe.

Friday, 15 April 2016

Tetemeko la ardhi laua 9 Japan

Takriban watu tisa wameuwa wakati wa tetemeko kubwa la ardhi lililokumba eneo la kusini mwa Japan siku ya Alhamisi.
Wengi wa waathiriwa ni kutoka mji wa Mashariki ambapo jengo moja liliporomoka na pia nyumba nyingi kuharibiwa.
Kote nchini, zaidi ya watu 40,000 waliondoka manyumbani mwao lakini baadhi yao wameanza kurudi licha ya kuwepo mitetemeko midogo midogo.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema kwa serikali imetuma polisi, wazema moto na wanajeshi kuendesha oparesheni za uokoaji.

Thursday, 14 April 2016

Wanasayansi wagundua dawa 'inayorefusha maisha'

Dawa inayotumika kwa matibabu ya kawaida huenda ikategua kitendawili cha kurefusha maisha na kuzuia uzee.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya, ambao ulibainisha kwamba viwango vya chini vya dawa aina ya Lithium vilisaidia kurefusha maisha ya nzi waliowekwa kwenye maabara.
Wanasayansi wamesema utafiti huu unatoa matumaini ya kutoa dawa kuwasaidia watu kuishi maisha marefu na yenye afya.
Lithium inatumika katika matibabu ya matatizo ya akili, kama mfadhaiko, na kusongwa na mawazo.
Hata hivyo ina madhara makubwa ikiwa itatumika kwa viwango vya juu.
Haijulikani jinsi Lithium inavyotibu matatizo ya akili, lakini alipopewanzi, dawa hiyo ilisaidia kurefusha maisha yao.
Hata hivyo watafiti wamesisitiza lazima dawa hii kutumiwa kwa viwango vya chini zaidi, kwani viwango vya juu vinaweza kuleta maafa.
Dkt Ivana Bjedov mmoja wa watafiti kutoka taasisi ya matibabu ya saratani amesema dawa hii itasaidia afya kwa wazee sawa na kuzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa kutetemeka 'Parkinson'.
Kando na matatizo ya akili Lithium imetumika kutibu maumivu makali ya kichwa 'Migraines' na ugonjwa wa jongo unaomfanya mtu kuvimba viungo hasa wakati wa baridi.

Barcelona yatupwa nje michuano ya Uefa

Klabu ya soka ya Barcelona Jumatano ilivuliwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Atletico Madrid huku Mabao yote ya Altletico Madrid yakifungwa na Antoine Griez-mann na bao la pili likifungwa kwa mara nyingine na Antoine kwa njia ya penalti .
Kwa matokeo hayo Atletico Madrid wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 3 -2 baada ya awali kufungwa 2-1 na Barcelona katika Uwanja wa Camp Nou.
Katika mchezo mwingine Bayern Munich imefakiwa kutinga nusu fainali baada ya kuitoa Benfica kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa jana .
Mabao ya Benfica yamefungwa na Raul Alonso Rodriguez na Anderson Souza Conceicao , na magoli ya Bayern Munich yakifungwa na Arturo Vidal na Thomas Muller .
Hivyo Atletico Madrid na Bayern Munich zinaungana na Real Madrid ya Hispania pamoja na Manchester City katika nusu fainali ambayo droo yake itapangwa siku ya Ijumaa.

Wednesday, 13 April 2016

Je unataka kulipwa mshahara mkubwa ?Soma utafiti

e unataka kulipwa mshahara mkubwa ?
Unahitaji kujifunza udaktari au maswala ya kiuchumi.
Utafiti wa mafunzo ya fedha IFS umeripoti kuwa wanafunzi waliosomea utabibu na maswala ya kiuchumi huwa na mshahara mkubwa zaidi baada ya kuhudumu kwa takriban miaka 10.
Wanaume wanaohitimu katika masomo hayo hujizolea takriban pauni elfu 55,utafiti huo umebaini.
Taaluma zenye faida kubwa
ShahadaMapato
Udaktari£ 55,000
Uchumi£ 42,000
Uhandisi na Teknolojia£ 31,200
Sheria£ 30,100
Sayansi£ 29,600
Elimu£ 29,600
Usanifu mijengo£ 28,600
Hisabati na Sayansi ya Kompyuta£ 26,800
Biashara£ 26,500
Sayansi ya Jamii£ 26, 200
Historia na Falsafa£ 26,500
Bayolojia£ 25,200
Kilimo£ 21,400
Habari na Mawasiliano£ 19,300

Ndege za Marekani zaua al shabab Somalia

Ndege za kivita za Marekani zisizokuwa na rubani zimewaua karibu wanamgambo 12 wa kundi la al-Shabab kusini mwa Somalia kwa mujibu wa afisa mmoja nchini Marekani.
Msemaji wa makao makuu ya ulinzi nchini Marekani Jeff Davis, alisema kuwa mashambulizi hayo ya angani, yaliendeshwa siku ya Jumatatu na Jumanne katika eneo lililo Kaskakzinia mwa mji wa bandario wa Kismayo.
Alisema kuwa mashambulizi hayo yalilenga ngome za al-shabab ambazo ziitajwa kuwa hatari kwa Marekani.

Watu 5 wauawa Ruyigi Burundi

Watu waliojihami kwa bunduki wamewaua watu watano na kuwajeruhi wengine saba walipofyatua risasi katika soko moja iliyoko Mashariki mwa eneno la Ruyigi nchini Burundi.
Hili ni shambulio la hivi karibuni katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na msururu wa mauaji.
Abdalla Hassan ambaye ni mkuu wa mkoa wa eneno hilo la Ruyigi ametaja mauaji hayo kuwa uhalifu wa kivita kwani waliwashambulia raia wasiokuwa na hatia wala silaha.
''Kama kweli hawa watu walikusudia kupigana si basi wangelikwenda kwenye kituo cha polisi ama cha jeshi wakashambulie?
Mbona wanawashambulia wananchi maskini ambao hata silaha hawana ,wamekosa nini ? aliuliza bw Hassan.

Tuesday, 12 April 2016

Mtu mrefu duniani awasili Mauritius



Mtu mrefu zaidi duniani raia wa Uturuki Sultan Kösen aliye na urefu wa futi 8 na inchi 3 au mita 2.51 amewasilia nchini Mauritius leo asubuhi.
Sultan alilakiwa na umati katika kisiwa hicho cha bahari ya Hindi, kwa mujibu wa taarifa zilizowekwa kwenye ukusara wa facebook wa mtandao wa habari wa nchi hiyo.

Maduka zaidi ya 150 yateketea Tanzania

Moto mkubwa umezuka na kuteketeza vibanda vya maduka zaidi ya 150 katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera magharibi mwa Tanzania. Moto huo ambao ulianza Jumatatu majira ya sa 2:00 usiku umeteketeza mali na bidhaa za aina mbalimbali kama mchele, sukari, nguo, simu, pamoja na bidhaa zingine.
Gloria Kilio ambaye alikuwa akiuza vyakula vya nafaka, amesema stoo zake zote tatu (3) za nafaka zimeungua, “Stoo zilikuwa na magunia ya unga, mchele na sukari lakini vyote vimeteketea,” amesema Gloria huku akilia. Anasema wakati moto unatokea alikuwa tayari amekwisha kwenda nyumbani na kuwaacha wafanyakazi wake wakimalizia kufunga vibanda.
Wafanyabiashara wengi wanasema walikuwa na mikopo na wengi wao hawana bima ya mali zao. Jonasi Nyarugenda ni miongoni mwa wafanyabiashara hao: “Moto umeteketeza stoo zangu nne zenye bidhaa mbalimbali kama sukari, mchele, ngano na mafuta,: anasema Jonas na kuongeza, “kwakeli ukitathimini kwa haraka siyo chini ya milioni 45 zimepotea.” Amesema kwamba alikuwa hana bima katika mkopo wake wa milioni 20 kutoka katika benki.
Hasara hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na ukosefu wa vifaa vya kuzima moto. Wananchi wa Karagwe imewapasa kusubiri gari la Zimamoto kutoka Bukoba Mjini (magari ya uwanja wa ndege) ambako ni kilomita 120 kufika karagwe mjini. Hata hivyo magari hayo yalikuta maduka mengi yamekwishateketea.
Diwani wa kata ya Kanoni wilaya karagwe Sabi Rwazo amesema tukio hilo limewastua na ni tukio la kwanza la moto kuunguza soko wilayani humo. Anasema tatizo la ukosefu wa gari la zima moto linachangiwa na uhaba wa fedha. “Mara nyingi katika bajeti yetu imekuwa ikishindwa kununua gari.” Amesema Rwazo na kusema maombi yao yako serikali kuu.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Deodatus Kinwiro amesema kuwa Serikali ya wilaya yake itapata gari la zima moto hivi karibuni, “Bahati nzuri nilikuwa Dar es Salaam, nimekutana na kamishna mkuu wa zima moto ameniahidi kunipatia gari jipya,” amesema Kinwiro na kuongeza kuwa, “wakati wowote gari hilo litafika wilayani Karagwe.”
Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema hawakubaliani na kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kwa sababu wamekuwa wakitozwa kiasi cha TZS 30,000 kwa mwezi ili kuchangia huduma za zimamoto wilayani hapo lakini wanashangaa kwa nini hawapati elimu ya kujikinga na majanga, na hakuna hata gari la dharura.
Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana lakini taarifa za awali zimeonesha kuwa kuna Mamalishe mwenye kibanda sokoni hapo aliacha jiko lake bila kuzima hivyo likashika nguo zilizokuwa katika kibanda hicho na kusababisha moto kusambaa ghafla.

Wafuasi wa Machar wachapwa vibaya Juba



Waasi nchini Sudan Kusini wanasema kuwa wanachama wake 16 wa kitengo cha habari, wamekamatwa na kupigwa vibaya na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba.
Kundi hilo la waandishi wa habari lilikuwa limetanguliwa katika mji mkuu wa Juba, siku kadhaa kabla ya kuwasili kwa kiongozi wa waasi Dkt Riek Machar.
Dkt Riek Machar anatarajiwa kutawazwa kuwa makamu wa rais kulingana na mkataba wa amani uliositisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyoanza Desemba mwaka wa 2013 kati ya waasi wanaomuunga mkono bw Machar na wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir.
Walikuwa wakijaribu kuwakusanya watu ili kumkaribisha naibu mwenyekiti vuguvugu la waasi, Alfred Ladu Gore